Jun 05, 2018 07:07 UTC
  • Jeshi la Nigeria lawaokoa watu 148 waliokuwa wakishikiliwa mateka na Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwakomboa watu 148, wakiwemo wanawake 58 na watoto 75, ambao walikuwa wametekwa nyara na kundi la magaidi wakufurishaji la Boko Haram.

Katika taarifa, Msemaji wa Jeshi la Nigeria Onyema Nwachukwu, amesema wanawake walionusuriwa walikuwa wanatumika kama watumwa wa ngono wa wapiganaji wa kundi hilo la magaidi wakufurishaji.

Watu hao wamekombolewa katika oparesheni maalumu iliyotekelezwa dhidi ya Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad katika eneo la mpakani la kaskazni mwa nchi hiyo katika Jimbo la Borno. Jeshi limesema oparesheni kali dhidi ya magaidi ingali inaendelea katika eneo hilo. 

Hivi karibuni Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa , UNICEF, ulisema tokea mwaka 2013 hadi sasa, magaidi wa Boko Haram wamewateka nyara  wasichana wadogo zaidi ya elfu moja katika maeneo ya kaskazkini na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Serikali ya Nigeria imekuwa ikikosolewa vikali kwa kuzembea katika kukabiliana na magaidi wa Boko Haram huku kukiwa na madai kuwa baadhi ya majenerali jeshini wanatajirika na uwepo wa kundi hilo la kigaidi.

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags