Waislamu Afrika Kusini walaani mauaji ya kikatili msikitini
Baraza la Kisheria la Waislamu la Afrika Kusini (MJC) limelaani vikali shambulizi la kikatili lililotokea Alhamisi katika eneo la Malmesbury karibu na mji wa Cape Town, na kusababisha vifo vya waumini wawili wa Kiislamu na wengine wawili kujeruhiwa.
Baraza hilo limesema mtu asiyejulikana aliingia msikitini na kujiunga na waumini kwenye sala ya usiku, baadaye alimvamia Imam na kumdunga kisu wakati akiswali, na kuwadunga kisu pia watu waliokwenda kumsaidia Imam huyo.
Kamishna Mkuu wa Polisi Bw Khehla Sitite ameiambia kamati ya usalama ya bunge, kuwa polisi na idara ya upelelezi wameanza uchunguzi kuhusu tukio hilo na wamelipa kipaumbele.
Mmoja kati ya waliouawa katika tukio hilo ametambuliwa kuwa Ismail Bassa aliyekuwa na umri wa miaka 72 na mke wake, Zainab Bassa, amesema mume wake ‘alichinjwa’ wakati alipokuwa akiswali. Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema aliyetekeleza hujuma hiyo alikuwa na asili ya Somalia.
Haya yanajiri mwezi mmoja tangu watu wanaosadikiwa kuwa magaidi wakufurishaji walipouvamia msikiti huo wa Imam Hussein AS karibu na mji wa Durban Afrika Kusini na kumuua shahidi Imamu wake kwa kumkata kichwa na kuwajeruhi waumini wengine kadhaa.
Magaidi hao waliokuwa na silaha mbali na kumuua Imamu wa msikiti waliwashambulia waumini kwa kuwadunga visu na kuwajeruhi kadhaa miongoni mwao.
Hakuna taarifa iwapo hujuma hizo mbili zinahusiana na hadi sasa hakuna kundi au mtu yeyote aliyedai kuhusika na mashambulizi hayo ya misikiti ambayo yamepelekea kuenea hofu katika jamii ya Waislamu Afrika Kusini.