Jun 16, 2018 07:21 UTC
  • Bemba awasili nchini Ubelgiji baada ya kuachiwa huru na ICC

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jean-Pierre Bemba, ambaye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC siku chache zilizopita ilimuondoa hatiani kuhusu jinai za kivita, amewasili nchini Ubelgiji baada ya kuachiliwa huru na mahakama hiyo.

Taarifa iliyotolewa na ICC imesema kuwa, Bemba ambaye amekuwa kizuizini kwa karibu miaka kumi, ameachiwa huru kwa muda na kwa masharti maalumu. Bemba anaaminika kujiunga na familia yake inayoishi katika eneo la Rhode-Saint-Genese, yapata kilomita 15 kusini mwa mji mkuu wa ubelgiji, Brussels, ambako alikamatwa Mei 2008, kufuatia ombi la ICC.

Bemba ameachiwa huru siku chache baada ya wakili wake, Melinda Taylor kutoa mwito kwa majaji wa ICC kumuamuru makamu huyo wa zamani wa Kongo DR ajiunge na familia yake nchini Ubelgiji.

Bemba, mwenye umri wa miaka 55, ambaye amekuwa katika kizuizi cha ICC tokea mwaka 2008 alipatikana na hatia ya kuhusika na jinai dhidi ya binadamu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani mwaka 2016.

Bemba ndani ya ICC

Mahakama hiyo ilisikiliza rufaa yake na kutoa hukumu Ijumaa illiyopita kwamba hana hatia na hivyo kutoa pigo kubwa kwa waendesha mashtaka.

Majaji wa rufaa walisema Bemba hawezi kubebeshwa lawama ya mauaji na ubakaji  wa raia uliofanywa na wanajeshi waliokuwa chini ya amri yake.

Bemba ambaye alikuwa makamu wa rais katika serikali ya mpito ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya Julai 2003 na Disemba 2006, alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2006 ambapo Kabila aliibuka mshindi.

Tags