Jun 27, 2018 13:38 UTC
  • Idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya kikabila Nigeria yapindukia 200

Gavana wa jimbo la Plateau lililoko katikati mwa Nigeria amesema idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya kikabila yaliyofanyika mwishoni mwa wiki imepindukia watu 200.

Simon Lalong ameyasema hayo leo Jumatano katika kikao na waandishi wa habari pambizoni mwa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo na kuongeza kuwa, mapigano hayo ya kikabila ni ya kutisha na yenye kutia wasiwasi mkubwa.

Ameongeza kuwa, kwa sasa serikali inakabiliwa na changamoto kubwa ya kujaribu kuwahifadhi na kuwapa misaada ya kibinadamu maelfu ya watu wengine ambao nyumba na mimea yao imeharibiwa kikamilifu kutokana na mapigano hayo ya kikabila.

Hapo awali  polisi ya Nigeria ilisema watu 86 wameuawa katika mapigano hayo yaliyotokea kwenye jimbo la Plateau la katikati mwa nchi hiyo, baina ya wakulima na wafugaji ambao si wakazi wa eneo hilo.

Wanigeria wakiandamana dhidi ya wafugaji makatili

Serikali ya Nigeria imetangaza hali ya hatari na kupiga marufuku watu kutoka nje katika jimbo hilo la Plateau kuanzia saa 12 jioni hadi 12 asubuhi kama ambavyo imetangaza serikali ya kijeshi katika eneo hilo katika juhudi zake za kujaribu kurejesha utulivu na hali ya kawaida.

Mapigano ya kikabila nchini Nigeria hutokea mara kwa mara na yamekuwepo kwa miongo kadhaa sasa ingawa yameongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni.

Tags