Jun 29, 2018 07:36 UTC
  • Watu 10 wauawa katika mapigano ya kikabila magharibi mwa Ethiopia

Watu wasiopungua kumi wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea magharibi mwa Ethiopia.

Shirika la habari la serikali la Fana liliripoti habari hiyo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, mbali na watu kumi kuuawa, wengine 56 wanauguza majeraha ya risasi na kukatwa kwa mapanga, kutokana na mapigano hayo yaliyotokea katika mji wa Assosa, eneo la Benishangul-Gumuz, magharibi mwa nchi.

Ashadli Hassen, mkuu wa eneo hilo amesema watu 40 wamekamatwa wakihusishwa na mauaji na machafuko hayo yaliyoanza tangu Jumatatu iliyopita.

Mashirika ya kutoa misaada ya kinadamu yamesema hali ya taharuki ingali imetanda katika eneo hilo, huku uhasama wa kikabila katika eneo hilo ukizidi kupanuka.

Waziri Mkuu wa Ethiopia

Wiki mbili zilizopita, watu 10 waliuawa katika mapigano mengine kati ya watu wa makabila ya Sidama na Wolaita katika mji wa Awasa kusini mwa nchi. Aidha watu wengine 89 walijeruhiwa huku wengine 500 wakilazimika kuwa wakimbizi. 

Wiki moja baada ya kuapishwa, Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia alizuru maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia machafuko nchini humo yaliyowalazimisha watu karibu milioni moja kuyahama makazi yao, ambapo aliahidi kutafuta suluhisho la kudumu la machafuko hayo katika muda mfupi sabamba na kuwasaidia wale wote waliolazimika kuyahama makazi yao.

Tags