Ban atahadharisha dhidi ya uchochezi na ubaguzi, kuepuka mauaji ya kimbari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4651-ban_atahadharisha_dhidi_ya_uchochezi_na_ubaguzi_kuepuka_mauaji_ya_kimbari
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ili kuzuia kutokea mauaji ya kimbari, lazima jamii zote duniani zijiepushe na uchochezi na matamshi ya chuki yanayoweza kuibua mfarakano na uhasama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 08, 2016 04:35 UTC
  • Ban atahadharisha dhidi ya uchochezi na ubaguzi, kuepuka mauaji ya kimbari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ili kuzuia kutokea mauaji ya kimbari, lazima jamii zote duniani zijiepushe na uchochezi na matamshi ya chuki yanayoweza kuibua mfarakano na uhasama.

Ban Ki-Moon ameyasema hayo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda mwaka 1994, iliyong’oa nanga hapo jana Alkhamisi. Moon amesema mauaji ya kimbari ni mchakato unaochukua muda mrefu na kuonya kuwa hakuna sehemu yoyote ya dunia yenye kinga ya kutofikiwa na jinamizi hilo; na hivyo kutoa wito wa kupewa adhabu kali wanaokumbatia uchochezi na kutoa matamshi ya chuki na kibaguzi.

Katibu Mkuu wa UN kadhalika amevitadharisha vyombo vya habari dhidi ya kueneza na kuwapa jukwaa wanaoshabikia uozo huo ambao unaweza kuitumbukia nchi yeyote ile katika matatizo makubwa. Aidha amezitaka nchi za Umoja wa Mataifa kuwakamata na kuwakabidhi kwa vyombo husika, watoro wengine waliohusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda ili wachukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huo huo, Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Spika wa Bunge la Seneti la Kenya Ekewe Ethuro ni miongoni mwa shakhsia waliotuma jumbe zao kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 22 ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda, kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame, familia za waathiriwa na Wanyarwanda wote wa ujumla.

Karibu watu milioni moja wengi wao wakiwa Watusti waliuawa katika mauaji hayo ya kimbari yaliyofanywa na Wahutu wenye misimamo mikali.