Jul 14, 2018 07:46 UTC
  • Bemba kugombea urais nchini Kongo baada ya kuachiwa huru na ICC

Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye hivi karibuni aliachiwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ameteuliwa na chama chake kugombea urais katika uchaguzi ujao nchini humo.

Chama chake cha Movement for the Liberation of Congo’s (MLC) kilimtangaza Jean-Pierre Bemba kuwa mgombea wake wa urais hapo jana Ijumaa katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu Kinshasa.

Bemba ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji, muda mfupi baada ya tangazo hilo alihutubia wafuasi wake kwa njia ya simu, na kuwaahidi kuwa atarejea nyumbani karibuni hivi.

Mwezi uliopita, Leonard She Okitundu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo DR aliamuandikia barua Spika wa Seneti ya nchi hiyo, akitaka Jean-Pierre Bemba apewe pasi ya kidiplomasia kupitia ubalozi wa DRC mjini Brussels na kuruhusiwa arejee nyumbani.

Bemba katika mahakama ya ICC

Bemba mwenye umri wa miaka 55, ambaye amekuwa katika kizuizi cha ICC tokea mwaka 2008 alipatikana na hatia ya kuhusika na jinai dhidi ya binadamu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani mwaka 2016, lakini aliachiwa huru hivi karibuni baada ya kukata rufaa kwenye kesi hiyo.

Uchaguzi mkuu nchini DRC unatazamiwa kufanyia Disemba 23 mwaka huu.

 

Tags