Jul 15, 2018 07:34 UTC
  • Askari 23 wa Nigeria watoweka baada ya shambulizi la Boko Haram

Wanajeshi wasiopungua 23 wa Nigeria hawajulikani walipo baada ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kushambulia msafara wa magari ya jeshi kaskazini mashariki mwa nchi.

Afisa wa jeshi ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, hatima ya wanajeshi 23 wakiwemo watano wa akiba haijulikani kufikia sasa, baada ya wanachama wa Boko Haram kuvizia na kuvamia msafara wa magari ya jeshi la nchi hiyo mjini Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno.

Amesema shambulizi hilo lilitekelezwa na wanachama zaidi ya 100 wa Boko Haram katika kijiji cha Balagallaye, eneo la Boboshe nje kidogo ya mji wa Bama.

Ameongeza kuwa, jeshi la Nigeria limepoteza magari yao manane katika hujuma hiyo.

Wanajeshi wa Nigeria

Mapema mwezi huu, magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani ya nchi, katika eneo la mpaka wa Nigeria na Cameroon, ambapo watu wasiopungua wanane waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009, huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

 

Tags