Jul 22, 2018 13:53 UTC
  • Boko Haram yaua watu 18 na kuteka nyara 10 Chad

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeshambulia kijiji kimoja kilichoko karibu na mpaka wa Chad na Niger, ambapo watu 18 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Gavana wa eneo la Ziwa Chad, Mohammed Aba Salah amewaambia waandishi wa habari leo Jumapili kwamba, mbali na kuua na kujeruhi, wanachama wa kundi hilo la ukufurishaji pia wamewateka nyara wanawake 10 katika hujuma hiyo.

Amebainisha kuwa, "Magaidi hao wameuawa watu wawili kwa kuwakata vichwa na 16 kwa kuwapiga risasi." Afisa huyo wa serikali ya Chad ameongeza kuwa, wakazi zaidi ya 3,000 wa eneo la Ziwa Chad wamelazimika kuyahama makazi yao baada ya magaidi hao wa kitakfiri kuvamia kijiji chao.

Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Ulinzi ya Nigeria imesema wanajeshi wa nchi hiyo wamefanikiwa kuwaangamiza wanachama 10 wa Boko Haram katika kijiji cha Baroua, eneo la Diffa, kusini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika magharibi.

Wapiganaji wa Boko Haram

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi watatu wameuawa na kujeruhiwa katika makabiliano makali yaliyotokea kati yao na magaidi hao katika kijiji hicho, kati ya Ijumaa na Jumamosi.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi yake tangu mwaka 2009 huko kaskazini mwa Nigeria ambapo katika hujuma hizo zaidi ya watu elfu 20 wa nchi hiyo na nchi jirani wameuawa. Aidha zaidi ya watu milioni mbili na laki sita pia wamekuwa wakimbizi.

Tags