Magaidi 87 wa al Shabab wauawa kusini mwa Somalia
Serikali ya Somalia imetangaza kuwa imewaangamiza magaidi 87 wa kundi la al Shabab katika mapigano yaliyotokea jana kusini mwa nchi hiyo.
Naibu Waziri wa Habari wa Somalia, Aden Isaaq Ali amesema kuwa, askari 5 wa jeshi la Somalia pia wamefariki dunia katika mapigano hayo yaliyotokea kwenye kambi ya jeshi ya eneo la Bar-Sanguni.
Amesema wapiganaji wa kundi la al Shabab walishambulia kambi hiyo kwa kutumia magari mawili yaliyokuwa na mabomu.
Mapema jana kundi la wanamgambo wa al Shabab lenye makao yake nchini Somalia lilikuwa limetangaza kuwa limeshambulia kambi moja ya jeshi kwa bomu lililotegwa garini huko kusini mwa nchi hiyo na kuuwa wanajeshi 27.
Shambulio hilo la kundi la al Shabab dhidi ya kambi ya jeshi nchini Somalia limefanyika baada ya lile la mwezi Juni mwaka huu ambapo kundi hilo pia lilishambulia kambi nyingine ya jeshi na kujeruhiwa wanajeshi saba wa Somalia. Al Shabab inadai kuwa inapigana kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali kuu ya Somalia.
Somalia ilitumbukia katika mapigano na machafuko ya ndani tangu ilipoondolewa madarakani serikali ya Mohamed Siad Barre mwanzoni mwa muongo wa 1990.