Kenya yaimarisha usalama wa wanaoendesha vita dhidi ya mafisadi
Serikali ya Kenya imemarisha usalama wa waendesha mashtaka, makachero na mashahidi wanaohusika katika kampeni mpya rasmi ya vita dhidi ya mafisadi nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Sunday Nation, serikali imechukua hatua maalumu kuimarisha usalama wa Mwendesha Mashtaka Mkuu (DPP) Noordin Haji ambaye anaongoza vita dhidi ya maafisa wa ngazi za juu serikalini ambao wamehusishwa na ufisadi.
Taarifa zinasema sasa ameongezewa idadi ya walinzi na ni vigumu kufika katika ofisi yake kutokana na hatua kali za usalama zilizochukuliwa.
Aidha Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti na makachero wengine wameongezewa walinzi.
Akizungumza Jumamosi, Rais Uhuru Kenya ameihakikishia Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) anaiunga mkono kikamilifu katika vita vyake dhidi ya ufisadi. Ametoa wito kwa maafisa wote husika kuimarisha mikakati ya kukabiliana na mafisadi na jinai za kiuchumi nchini humo. Aidha ametaka taasisi zote husika za serikali zishirikiane ili kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.