Wakulima Afrika Kusini: Trump! Tuache tupumue!
Wakulima nchini Afrika Kusini wamekasirishwa na matamshi ya kichochezi ya rais wa Marekani, Donald Trump na kumtaka asijiingize katika mambo yasiyomuhusu.
Shirika la habari la AFP limewanukuu wakulima wa Afrika Kusini wakionesha hasira zao hizo baada ya Donald Trump kudai kuwa ana wasiwasi na marekebisho hayo ya mashamba.
Kwa mujibu wa AFP, wakulima wote wa Afrika Kusini, Wazungu na Waafrika wamezungumza na vyombo vya habari na kumtaka rais huyo wa Marekani asijiingize katika mambo yasiyomuhusu na asijaribu kueneza fitna huko Afrika Kusini.
Shirika hilo la AFP la nchini Ufaransa limewanukuu wakulima hao wa Afrika Kusini wakisema: Trump! Tuache tupumue!
Siku ya Jumatano, rais wa Marekani, Donald Trump alidai kuwa serikali ya Afrika Kusini inafanya njama za kupora ardhi za Wazungu na alimtaka Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani alifuatilie kwa karibu zoezi la marekebisho ya mashamba nchini Afrika Kusini.
Viongozi wa Afrika Kusini walijibu haraka uchochezi huo wa Trump na kusema kuwa rais huyo wa Marekani alikuwa anapotosha na amekusudia kueneza fitna nchini Afrika Kusini. Nchi hiyo ilimwita balozi wa Marekani mjini Pretoria na kumkabidhi malalamiko yake makali kutokana na matamshi hayo ya kuchochea ugomvi ya Trump.
Wakulima wa Afrika Kusini nao, Wazungu na Waafrika, wote wamekasirishwa sana na uchochezi wa rais huyo wa Marekani na kumuonya asieneze fitna na asiingilie mambo yasiyomuhusu.