Watu 16 wauawa katika shambulio la waasi mashariki mwa DRC
(last modified Sun, 23 Sep 2018 16:00:29 GMT )
Sep 23, 2018 16:00 UTC
  • Watu 16 wauawa katika shambulio la waasi mashariki mwa DRC

Watu 16 wameuawa katika shambulio jipya la waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru za kuamika za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimetangaza leo kuwa waasi wa Uganda wa kundi la ADF wamefanya mauaji hayo katika mji wa Beni makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Daktari mmoja wa hospitali ya eneo hilo amesema kuwa ameona miili 16 ya watu waliouawa wakiwemo raia 12 na wanajeshi au waasi wanne. Watu wengine wanane wamejeruhiwa wakiwemo raia watano katika shambulio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo Jumapili. 

Waasi wa Ugada wa ADF wanaofanya mashambulizi yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 

Wafanyakazi wa kigeni wanaotoa misaada ya kibinadamu wako mjini Beni karibu na mpaka wa Uganda tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti ulipozuka ugonjwa wa Ebola katika eneo hilo. Daktari huyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu wanne waliouawa katika shambulio hilo la kushitukiza walikuwa kwenye gari ya abiria. Watu walioshuhudia wamesema kuwa milio ya risasi ilisikika kwa masaa kadhaa hata alfajiri ya kuamkia leo.

Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Kongo yamekumbwa na machafuko kwa miaka 20 sasa.

Kushindwa jeshi la serikali na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kukabiliana na waasi ni moja ya sababu za kuendelea ukosefu wa amani na machafuko huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.