Rais Shein afungua maonyesho ya utalii Zanzibar ya mwaka 2018
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48865-rais_shein_afungua_maonyesho_ya_utalii_zanzibar_ya_mwaka_2018
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa, maonyesho ya utalii yanayofanyika Zanzibar ni muhimu kwa Serikali na wananchi kwa kuwa yamelenga kuitangaza Zanzibar na sekta ya utalii ambayo ndio mhimili mkuu wa uchumi wa visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 17, 2018 15:14 UTC
  • Rais Shein afungua maonyesho ya utalii Zanzibar ya mwaka 2018

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa, maonyesho ya utalii yanayofanyika Zanzibar ni muhimu kwa Serikali na wananchi kwa kuwa yamelenga kuitangaza Zanzibar na sekta ya utalii ambayo ndio mhimili mkuu wa uchumi wa visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi.

Dk. Shein ameyasema hayo leo Mtoni Mjini Unguja katika ufunguzi wa maonyesho ya utalii Zanzibar ya mwaka 2018 ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, wadau wa utalii na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na wananchi.

Rais Shein amesema katika hafla hiyo kwamba, utalii umekuwa ukichangia asilimia 27 kwa Pato la Taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazokusanywa ambapo muda wanaokaa watalii visiwani Zanzibar umeongezeka kiasi kwamba hivi sasa mtalii hutumia wastani wa siku 8 badala ya 6 kama ilivyokuwa miaka 5 iliyopita.

Rais wa Zanzibar akisalimiana na Bi Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelezea juhudi mbalimbali za kuimarisha utalii zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zikiwemo kuanzisha mpango wa “Utalii kwa Wote” ambapo lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kwamba, sekta ya utalii inawanufaisha wakazi wote wa Zanzibar na kuimarisha ustawi wa wananchi kwa jumla. Kwa upande wake, Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar amesema kuwa, wizara yake imo katika hatua za kuhakikisha inavuka lengo la kufikia watalii nusu milioni kwa mwaka na kueleza kwamba, lengo hilo litavukwa kwani alithibitisha kuwa hadi Julai mwaka huu walifikia watalii 263,000 na kama kasi hiyo itaendelea basi mwisho wa mwaka huu watafikia watalii 520,000.