Oct 21, 2018 23:19 UTC
  • Matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Cameroon kutangazwa leo

Matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais uliofanyika Oktoba 7 nchini Cameroon yanatazamiwa kutolewa leo Jumatatu.

Baraza la Katiba, chama tawala CPDM na Tume ya Uchaguzi nchini humo Elecam zimesema uchaguzi huo umepasi viwango vyote vya demokrasia licha ya malalamiko ya hapa na pale ya vyama vya upinzani. 

Matokeo yasiyo rasmi yalidokeza kuwa, Rais Paul Biya ambaye aliwania kuendelea kubaki madarakani kwa kipindi kingine cha saba ambacho kitamfanya awe mmoja wa viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika ataibuka mshindi wa uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 71 ya kura. 

Hivi karibuni, Mahakama ya Katiba ya Cameroon ilitoa uamuzi wa kutupilia mbali kesi zote 18 zilizowasilishwa na wapinzani kutaka uchaguzi huo urejewe kwa madai kwamba ulitawaliwa na mizengwe na udanganyifu wa kumfungulia njia rais wa sasa Paul Biya mwenye umri wa miaka 85 kuendelea kuitawala nchi hiyo baada ya miaka 36 ya kuweko madarakani.

Kinara wa chama cha upinzani cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC), Maurice Kamto

Madai ya wapiga kura kutishwa na kutokea fujo na machafuko ni miongoni mwa sababu zilizowafanya wagombea wakuu watatu wa upinzani pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri kutoa wito wa kufutwa matokeo ya uchaguzi.

Itakumbukwa kuwa, Oktoba 9, mgombea wa chama cha upinzani cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC), Maurice Kamto alijitangaza mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Jumapili ya tarehe 7 Oktoba.

Tags