Oct 22, 2018 15:50 UTC
  • ICC yasikiliza kesi ya kamanda wa waasi wa Uganda wa LRA

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imeanza kusikiliza kesi ya kamanda wa genge la kigaidi la Kikristo la LRA lililokuwa linapigania kusimamisha serikali itakayoongozwa kwa amri kumi za Biblia nchini Uganda.

Kamanda huyo anahusishwa na mauaji ya watu laki moja. Hata hivyo wachunguzi wa mambo wanahoji ni kwa nini ni waasi tu ndio wanaopandishwa kizimbani na kufunguliwa mashtaka wakati pande zote mbili zilihusika katika mauaji kwenye mapigano hayo ya ndani nchini Uganda.

Televisheni ya Aljazeera ya Qatar imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, kesi ya kamanda huyo wa zamani waasi wa LRA anayejulikana kwa jina la Dominic Ongwen imeanza kusikilizwa katika mahakama ya ICC huku akikabiliwa na mashtaka 70 yakiwemo ya jinai za kivita na mauaji.

Waasi wa LRA

 

Kundi la waasi aliloliongoza kamanda huyo linahusishwa na vifo vya watu laki moja na kutekwa watu 20,000 wakiwemo watoto wadogo katika vita vya ndani vya miaka 20 nchini Uganda.

Televisheni hiyo aidha imesema, pamoja na kwamba pande zote mbili zinatuhumiwa kuhusika katika unyanyasaji na vitendo viovu, lakini ni viongozi wa waasi tu ndio wanaopandishwa kizimbani huko ICC, jambo ambalo linawafanya Waganda wengi wajiulize je, hii ni kesi ya washindi tu na haiwahusu watu wengine wengi waliohusika katika ukatili uliofanyika kwenye vita hivyo ambavyo ni moja ya vita vibaya zaidi barani Afrika? 

Tags