Sudan yaondoa marufuku ya uingizaji mazao ya kilimo kutoka Misri
Rais Omar al Bashir wa Sudan jana alitoa dikrii na kuondoa marufuku ya miezi 17 ya kuzuia kuingizwa nchini humo mazao ya kilimo kutoka Misri.
Bidhaa muhimu ambazo zinaingizwa Sudan kutoka Misri ni pamoja na matunda, mboga, samaki, bidhaa za makopo na zile za nguo. Jana Alhamisi nchi mbili hizo zilisaini hati 12 za makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Tarehe 19 mwezi Machi mwaka huu Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri na mwenzake wa Sudan, Omar Hassan al Bashir walikutana na kukubaliana kuboresha uhusiano wa nchi mbili hizo baada ya miezi kadhaa ya mivutano kati ya Cairo na Khartoum.
Uhusiano wa nchi mbili za Sudan na Misri ulitumbukia katika hali ya mivutano mwanzoni mwa mwaka jana baada ya Rais wa Sudan kuituhumu Misri kuwa inayaunga mkono makundi ya waasi katika maeneo yaliyokumbwa na vita huko Sudan likiwemo jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo.
Mwezi Mei mwaka jana Sudan ilipiga marufukuu uingizaji wa wanyama na bidhaa za kilimo kutoka Misri na mwezi Januari mwaka huu ikimrejesha nyumbani balozi wake kutoka Cairo.