Nov 12, 2018 07:46 UTC
  • Mamia ya raia wakimbia baada ya shambulio la Boko Haram Nigeria

Mamia ya wanavijiji juzi jioni walizikimbia nyumba zao huko kaskazini mashariki mwa Nigeria baada ya wanamgambo wa kundi la Boko Haram kuwashambulia.

Hakuna mtu yoyote aliyeripotiwa kuuawa hata hivyo kujiri shambulio hilo kunaashiria kulegalega kwa hali ya usalama huko kaskazini mashariki mwa Nigeria ambako jeshi la nchi hiyo lingali linaendesha mapambano dhidi ya hujuma za kundi hilo zilizoanza mwaka 2009.    

Watu walioshuhudia wameeleza kuwa wanamgambo wa Boko Haram waliwasili juzi jioni huko Jimmi umbali wa kilomita 5 kutoka mji wa Maiduguri na kuanza kufyatua risasi na kuchoma nyumba na vile vile kushambulia kambi ya wakimbizi isiyo rasmi katika eneo hilo. Musa Ari ambaye ni mmoja wa watu walioshuhudia shambulio hilo huko Maiduguri  amesema kuwa magaidi wa Boko Haram juzi jioni walikishambulia kijiji cha Jimmi na kuanza kuchoma nyumba za raia na mahema ndani ya kambi hiyo ya wakimbizi.

Mali za raia zilizochomwa moto kambini na magaidi wa Boko Haram huko Maiduguri

Wanavijiji waliojawa hofu walikimbilia katika eneo jirani ambalo ni makao makuu ya jimbo la Borno ili kuepa shambulio hilo la Boko Haram. Wakati huo huo jeshi la Nigeria lilijaribu kujibu shambulio hilo la magaidi wa Boko Haram kwa kutumia helikopta za kijeshi ambazo zilionekana zikipaa kuelekea katika kijiji cha Jimmi. Katika miezi ya karibuni kundi hilo la kigaidi limefanya mashambulizi makubwa katika kambi za jeshi na kuua raia pia licha ya serikali ya Nigeria kusisitiza kwamba wanamgambo wa Boko Haram wanakaribia kusambaratishwa.  

 

Tags