Nov 13, 2018 02:52 UTC
  • Makumi ya watu waripotiwa kuaga dunia Nigeria kwa kipindupindu

Kamisheni ya Wakimbizi ya Norway imetangaza kuwa idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu yameshika kasi zaidi huko kaskazini mwa Nigeria ambako makumi ya maelfu ya raia wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yanayofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Jumuiya hiyo ya misaada ya kibinadamu imetangaza kuwa, watu elfu kumi wameathiriwa na ugonjwa huo na 175 kati yao wameaga dunia katika majimbo ya kaskazini mwa Nigeria ya Adamawa, Borno na Yobe.

Mkurugenzi wa Mipango wa Norwegian Refugee Council, Janet Cherono amesema kuwa, miongoni mwa sababu zinazochangia maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo hayo ni msongamano mkubwa katika kambi za wakimbizi unaotatiza suala la kufikishwa maji kwa wahitaji, usafi wa mazingira na huduma za afya.

Kipindupindu kimeua zaidi ya watu 170 kaskazini mwa Nigeria.

Cherono ameongeza kuwa, msimu wa mvua kali pia umezidisha hali mbaya kwa wakimbizi wa maeneo hayo na kwamba kuna udharura wa kujengwa vituo zaidi vya afya la sivyo Nigeria itakabiliwa na wimbi kubwa na maambukizi ya kipindupindu katika mwaka ujao wa 2019.

Karibu Wanigeria milioni mbili wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanachama wa kundi la Boko Haram.

Zaidi ya watu elfu 27 wameuawa katika mashambulizi hayo yaliyoanza mwaka 2009.  

Tags