Nov 20, 2018 08:04 UTC
  • Jeshi la Nigeria lakosolewa kwa 'kumuua mara mbili' kamanda wa Boko Haram

Waandishi wa habari, wakosoaji wa serikali na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Nigeria wamelijia juu jeshi la nchi hiyo kwa kutangaza kuwa limemuua kamanda mwandamizi wa kundi la kigaidi la Boko Haram, licha ya kutoa taarifa kama hiyo mwaka jana.

Ukosoaji huo umefuatia ufichuzi uliofanywa na mwandishi mashuhuri wa habari za eneo la Ziwa Chad, Ahmed Salkida, ambaye ameandika kuwa ni fedheha kwa jeshi kutangaza 'kumuua mara mbili' kiongozi wa Boko Haram. Siku ya Jumamosi jeshi hilo lilitoa taarifa na kusema limefanikiwa kumuangamiza Baban Hassan, mkuu wa propaganda na mitandao ya kijamii ya Boko Haram.

Mwandishi huyo wa habari hata hivyo ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, "Jeshi la Nigeria lilitangaza kumuua Baban Hassan Ijumaa usiku, tarehe 3 Novemba mwaka jana 2017, iweje ameuawa tena Novemba mwaka huu?"

Jeshi la Nigeria lilitoa taarifa ya kuuawa kamanda huyo wa Boko Haram, ili kupunguza ghadhabu za wananchi wanaodai kuwa serikali imeshindwa kukabiliana na genge hilo la ukufurishaji.

Wanamgambo wa Boko Haram

Siku chache kabla ya hapo, kundi hilo la ukufurishaji lilishambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua wakulima wasiopungua 16.

Licha ya serikali ya Nigeria kutangaza mwishoni mwa mwaka 2015 kuwa Boko Haram limesambaratishwa kwa kiasi kikubwa, lakini kundi hilo lingali lina uwezo wa kufanya mashambulizi katika mji wa Maiduguri, maeneo ya karibu yake na katika maeneo mengi ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.  

Tags