Dec 07, 2018 14:39 UTC
  • Raia 17 wauawa katika mashambulizi ya ADF Kongo DR

Raia wasiopungua 17 wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na kundi la wanamgambo wa ADF mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Meya wa mji wa Beni, Nyonyi Masumbuko Bwanakana ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, 12 miongoni mwao waliuawa jana Alkhamisi katika mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa ADF wa Uganda katika eneo la Mangolikene, nje kidogo ya mji wa Beni, eneo la Kivu Kaskazini.

Ameongeza kuwa, raia wengine watano wameuawa na wapiganaji hao wa ADF usiku wa kuamkia leo katika eneo la Paida, katika mkoa huo huo wa Kivu Kaskazini.

Kapteni Mak Hazukay, msemaji wa jeshi la Kongo DR katika eneo hilo amesema operesheni ya kuwasaka wanamgambo wa ADF waliotekeleza hujuma hizo za kigaidi inaendelea.

Askari wa serikali ya DRC eneo la Kivu Kaskazini

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu wengine 18 kuuawa katika mapigano kati ya jeshi na waasi watiifu kwa Jenerali muasi wa zamani wa jeshi William Amuri Yakutumba, katika eneo la Fizi katika mkoa tajiri kwa madini wa Kivu Kusini huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mauaji na mashambulizi hayo yanajiri katika hali ambayo, kampeni za uchaguzi zinaendelea kushika kasi katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu nchini humo uliopangwa kufanyika Desemba 23. 

Tags