Nigeria yaitimua UNICEF kwa tuhuma za kuwapa mafunzo majasusi wa Boko Haram
(last modified Sat, 15 Dec 2018 07:01:11 GMT )
Dec 15, 2018 07:01 UTC
  • Nigeria yaitimua UNICEF kwa tuhuma za kuwapa mafunzo majasusi wa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limesimamisha shughuli za Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) katika eneo la kaskazini mashariki kwa nchi, kwa tuhuma kuwa maafisa wake wanawapa mafunzo na kushirikiana na majasusi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Hraram.

Katika taarifa ya jana Ijumaa, jeshi hilo limedai kuwa UNICEF iliandaa warsha tarehe 12 na 13 mwezi huu katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, na eti 'kuwapa mafunzo watu fulani kwa ajili ya shughuli fulani,' jambo ambalo linahatarisha na kuvuruga operesheni za jeshi hilo dhidi ya Boko Haram.

Taarifa hiyo ya jeshi la Nigeria imedai kwamba,  "UNICEF imekuwa ikiwapa mafunzo watu fulani, kwa lengo la kuyumbisha jitihada za kupambana na ugaidi, kwa kuwazushia tuhuma za ukiukaji wa haki binadamu wanajeshi wa Nigeria."

Wanamgambo wa Boko Haram

Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Kanali Onyema Nwachukwu, imeongeza kuwa, UNICEF inawapa mafunzo majasusi ambao wanawaunga mkono wanamgambo na hivyo kuhatarisha vita dhidi ya ugaidi, na kwa msingi huo, Kamandi Kuu ya Operesheni za LAFIYA DOLE (za kupamabana na Boko Haram) zimesimamisha kazi za UNICEF kaskazini mashariki mwa nchi, hadi maelezo mengine yatakapotolewa.

Boko Haram ni kundi linalofuata itikadi za Kiwahhabi na limeitumbukiza Nigeria katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha mizozo ya kidini na kikabila katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009.