Dec 16, 2018 02:45 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Tuna wasiwasi na hali ya wakimbizi DRC

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeelezea wasiwasi mkubwa lilionao kuhusiana na hali mbaya wanayokabiliwa nayo wakimbizi zaidi ya milioni moja katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Charlie Yaxley, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)  amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kwamba, kutokana na kuendelea mapigano na vitendo vya utumiaji mabavu katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, umoja huo umeshindwa kuyafikia maeneo kadhaa yaliyokumbwa na mapigano  na hivyo kutoweza kuwafikishia misaada ya kibinadamu wakazi wa maeneo hayo.

Afisa huyo wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa, raia wengi wa maeneo yanayokabiliwa na machafuuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanahitajia misaada ya kibinadamu.

Charlie Yaxley, aidha amesema kuwa, kutokuwa na nyumba, sehemu za kujihifadhi, kukosekana vyanzo vya chakula cha kutosha na uhaba wa huduma nyingine muhimu ni mambo ambayo yameifanya hali ya wakimbizi hao mashariki mwa nchi hiyo kuzidi kuwa mbaya.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuchunguza na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu sababu na chimbuko la kuzuka wimbi la wakimbizi katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na kuwasaidia pia wahanga wa mapigano na machafuko katika nchi hiyo.

Tags