Uchaguzi Madagascar; Ravalomanana apinga ushindi wa Rajoelina mahakamani
(last modified Fri, 28 Dec 2018 16:02:04 GMT )
Dec 28, 2018 16:02 UTC
  • Uchaguzi Madagascar; Ravalomanana apinga ushindi wa Rajoelina mahakamani

Siku moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Madagascar kutangaza matokeo ya muda yaliyoonesha kuwa rais wa zamani wa nchi hiyo Andry Rajoelina ndiye aliyepata kura nyingi zaidi katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyofanyika Disemba 19, mpinzani wake mkuu Marc Ravalomanana ameenda mahakamani kupinga matokeo hayo.

Tsehenoarisoa Rabenja, mkurugenzi wa timu ya kampeni ya Ravalomanana amesema "Tumewasilisha faili la kupinga matokeo hayo yaliyopikwa kwa maslahi ya Rajoelina katika Mahakama Kuu ya Katiba."

Ameongeza kuwa, "Usidhani kwamba tumesalimu amri, kulikuwako na udanganyifu na uchakachuaji wa matokeo. Kuna njama zilifanywa kabla ya uchaguzi wenyewe."

Kwa mujibu wa tume hiyo, Andry Rajoelina, ameshinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 55.66 ya kura, huku Marc Ravalomanana akipata asilimia 44.34 ya kura.

Kabla ya kutangazwa matokeo hayo ya muda, marais hao wa zamani wa Madagascar kila mmoja alijitangaza mshindi wa uchaguzi huo, siku moja baada ya zoezi hilo la Disemba 19. 

Rajoelina (kushoto) na Ravalomanana

Kwa upande wake, Rajoelina mwenye umri wa miaka 44, na ambaye aliwahi kuwa meya wa mji mkuu Antananarivo mwaka 2007 na aliongoza nchi kwa miaka 5, kuanzia 2009 hadi 2013, amewataka wananchi kuwa watulivu, huku akitupilia mbali madai hayo ya wizi wa kura.

Mahakama Kuu ya Katiba ina siku tisa kuanzia jana Alkhamisi, kuthibitisha matokeo hayo ya muda yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa bara Afrika.