Jan 10, 2019 08:11 UTC
  • Wanigeria zaidi ya elfu 30 wakimbia makazi yao kaskazini mwa nchi hiyo

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia nyumba na makazi yao huko kaskazini mwa Nigeria kutokana na kushadidi ghasia na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Edward Kallon amesema kuwa, katika wiki za hivi karibuni zaidi ya wakimbizi elfu 30 wengi wao wakitokea eneo la Baga wamewasili katika eneo la Maiduguri huko kaskazini mashariki mwa Nigeria kutokana na mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa na  afisa huyo wa Umoja wa Mataifa imesema mapigano makali yaliyotokea baina ya jeshi la Nigeria na makundi ya waasi karibu na Ziwa Chad mwishoni mwa mwezi uliopita yamewalazimisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kusababisha maafa makubwa ya kibinadamu. 

Mapigano hayo pia yamewalazimisha wafanyakazi 260 wa misaada ya kibindamu kukimbia maeneo yaliyoathiriwa tangu mwezi Novemba mwaka jana katika kile kinachotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni operesheni kubwa zaidi ya kuondoka wafanyakazi wa misaada ya kibindamu katika maeneo yaliyoathiriwa tangu mwaka 2016.  

Muhammadu Buhari

Mashambulizi ya sasa ya kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria yanatoa changamoto kubwa kwa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo aliyeahidi kulitokomeza kundi hilo katika kampeni za uchaguzi wa rais uliomfikisha madarakani. Buhari ameteuliwa na chama tawala kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi ujao.  

Tags