UN: 13 wauwa kabla ya kuanza mazungumzo ya kusaka amani CAR
(last modified Wed, 23 Jan 2019 07:48:30 GMT )
Jan 23, 2019 07:48 UTC
  • UN: 13 wauwa kabla ya kuanza mazungumzo ya kusaka amani CAR

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa watu 13 wameuawa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, siku chache kabla ya kuanza duru mpya ya mazungumzo ya amani kati ya serikali na makundi ya upinzani.

Vladimir Monteiro, msemaji wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (Minusca) amesema watu hao waliuawa Jumapili iliyopita baada ya watu waliobeba silaha wa kabila la Fulani kushambulia kijiji cha Zaoro Sangou, magharibi mwa nchi.

Wakazi wa kijiji hicho wanasema wanachama wa kundi la 3R linalodai kupigania maslahi ya jamii ya Fulani waliingia kijijini hapo na kuanza kufyatua risasi ovyo na kuua watu 13 na kujeruhi wengine wengi.

Kundi hilo ni miongoni mwa makundi ya kisiasa ambayo yanatazamiwa kushiriki mazungumzo mapya ya amani.

CAR ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani

Mazungumzo hayo ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati  na makundi 14 ya upinzani imepangwa kufanyika kesho (Januari 24) mjini Khartoum, Sudan.

Mazungumzo hayo, yanayosimamiwa na Umoja wa Afrika, yanalenga kushughulikia masuala ya utawala wa serikali, msamaha, wapiganaji kurudi katika jamii na ushiriki wa vyama vya siasa kwenye utawala, katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika ambayo ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013, baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka.