Jan 24, 2019 04:06 UTC
  • Wimbi jipya la wakimbizi laibuka kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia kuongezeka machafuko

Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, kufuatia kuongezeka machafuko kaskazini mashariki mwa Nigeria, kwa mara nyingine tena makumi ya maelfu ya raia wamelazimika kuwa wakimbizi katika maeneo hayo.

Farhan Haq, msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari kwamba, kwa mujibu wa taarifa walizopokea kutoka kwa asasi amilifu katika masuala ya kibinadamu, watu wasiopungua 80,000 wamelazimika kuwa wakimbizi kuanzia Novemba mwaka jana hadi sasa baada ya kuibuka mapigano mapya baina ya makundi ya wabeba silaha na jeshi la Nigeria kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika hususan katika jimbo la Borno.

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa  ameongeza kuwa, idadi hii inawafanya watu waliolazimika kuwa wakimbizi hadi sasa kaskazini mashariki mwa Nigeria kufikia milioni moja na laki nane.

Farhan Haq, msemaji wa Umoja wa Mataifa

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, umoja huo na taasisi amilifu katika masuala ya kibinadamu zimeonyesha wasiwasi mkubwa zilionao kuhusiana na kushadidi machafuko na ukosefu wa amani kabla na baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Nigeria tarehe 16 ya mwezi ujao wa Februari pamoja na vizingiti vya ufikishaji misaada ya kibinadamu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Farhan Haq amezitaka pande zote zinazopigana nchini Nigeria kuwalinda raia na kuheshimu sheria za kimataifa.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu milioni saba wanahitajia misaada ya kibinadamu kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tags