Feb 02, 2019 12:41 UTC
  • Amnesty: Boko Haram imeua watu 60 kaskazini mwa Nigeria

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema watu wasiopungua 60 wameua na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Osai Ojigho, Mkurugenzi wa shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London amesema kuwa, shambulizi hilo la Boko Haram lilifanyika Jumatatu iliyopita katika mji wa Rann, katika jimbo la Borno.

Ameitaja hujuma hiyo kama baya zaidi kuwahi kufanywa na magaidi hao wakufurishaji katika miaka ya hivi karibuni.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Umoja wa Mataifa ulisema watu zaidi ya 30,000 wamekimbia makazi yao katika mji wa Rann kaskazini mwa Nigeria na kuingia katika nchi jirani ya Cameroon kutokana na wasiwasi wa kushambuliwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Ramani ya Nigeria inayoonesha jimbo la Borno

Machafuko na ukosefu wa amani vinashuhudiwa katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa tarehe 16 ya mwezi huu wa Februari. Aidha kuna vizingiti vya ufikishaji misaada ya kibinadamu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa UN, zaidi ya watu milioni saba wanahitajia misaada ya kibinadamu kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tags