Afrika Kusini ina hamu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Iran
Spika wa Bunge la Kitaifa la Afrika Kusini ameeleza juu ya utayarifu wa nchi yake wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baleka Mbete aliyasema hayo jana Alkhamisi mjini Cape Town katika mazungumzo yake na Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa.
Pamoja na masuala mengine, wawili hao wamezungumzia pia kuhusu umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kisiasa wa nchi mbili hizi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa yuko nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kufanyika duru ya tisa ya mazungumzo ya Kamati ya Kisiasa ya Jamhuri ya Kiislamu na Afrika Kusini.
Mbali na kumpa salamu kutoka kwa mwenzake wa Iran, Ali Larijani, Araqchi amemtaarifu Spika wa Bunge la Kitaifa la Afrika Kusini kuhusu hali ya hivi sasa ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na mfumo wa mabadilishano ya kifedha wa Umoja wa Ulaya utakaoyawezesha mabenki kuwa na ushirikiano na Iran licha ya kuwepo vikwazo vya Marekani.
Afrika Kusini ni nchi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa barani Afrika na imekuwa ikichukua hatua chanya za kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa baada ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Vika Mazwi Khumalo, Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran alisema hatua ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA haitapunguza ushirikiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga za uchumi, biashara na utamaduni.