Barabara ya kwanza ya juu (flyover) kujengwa Dar-es-Salaam Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela, eneo la Tazara Jijini Dar es salaam ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2018.
Barabara hiyo ya juu itakuwa ya kwanza kujengwa nchini Tanzania na ujenzi wake unatarajiwa kugharimu kiasi cha takribani shilingi Bilioni 100 ambapo kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 93.44 zitatolewa na Japan kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA), na Serikali ya Tanzania itatoa shilingi Bilioni 8.3.
Barabara ya juu itakayojengwa itakuwa na njia nne na urefu wa mita 300 kutokea maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es salaam kuelekea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, na inatarajiwa kupunguza kero ya msongamano wa magari yanayoenda na kutoka uwanja wa ndege na bandari ya Dar es salaam. Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Rais John Pombe Magufuli amesema barabara hiyo inajengwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya serikali yake ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari Jijini Dar es salaam. Rais Magufuli amebainisha juhudi nyingine za kukabiliana na msongamano wa magari Jijini Dar es salaam kuwa ni pamoja na kujenga barabara ya njia sita ya Dar es salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na Flyover tano, ujenzi wa barabara nyingine za juu katika makutano ya barabara za Nelson Mandela, Morogoro na Sam Nujoma eneo la Ubungo na ujenzi wa daraja jipya la Salander lenye urefu wa kilometa 6.23 kuanzia Coco Beach hadi hospitali ya Agha Khan.