Sudan na Sudan Kusini zakubaliana kufungua tena kivuko cha mpakani
Kamati ya usalama wa kisiasa ya pamoja kati ya Sudan na Sudan Kusini imeafiki suala la kufungua tena kivuko cha mpakani kati ya nchi mbili hizo.
Wajumbe wa kamati hiyo katika kikao chao cha jana huko Khartoum mji mkuu wa Sudan walisaini makubaliano kwa ajili ya kufungua tena kivuko cha mpakani kati ya nchi mbili hizo. Kamal Abdulmaaruf, mkuu wa vikosi vya majeshi ya Sudan amesema baada ya kikao hicho cha usalama kwamba: Imeamuliwa kuwa wanajeshi wanapasa kuondolewa kwa muda wa mwezi mmoja katika eneo la amani ili kuruhusu kutumwa timu ya pamoja chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Abyei na hivyo kupata hakikisho la kuondoka wanajeshi katika eneo hilo.
Sudan na Sudan Kusini Septemba 27 mwaka 2012 zilisaini makubaliano ya pamoja ya kiusalama ili kuzuia kutumwa silaha na zana za kijeshi mwa makundi ya waasi kupitia mipakani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, imeafikiwa kujengwa eneo lenye usalama la ukubwa wa kilomita kumi katika pande mbii za mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.
Nchi mbili hizo Septemba 27 mwaka juzi pia zilikubaliana kufungua tena vivuko vitatu vya pamoja vya mpakani kwa lengo la kuhuisha biashara, kuongeza uzalishaji wa mafuta na kukabiliana na magendo ya bidhaa.