Milipuko ya mabomu na milio ya risasi vyautikisa mji wa Mogadishu Somalia
(last modified Sat, 23 Mar 2019 14:15:42 GMT )
Mar 23, 2019 14:15 UTC
  • Milipuko ya mabomu na milio ya risasi vyautikisa mji wa Mogadishu Somalia

Duru za habari nchini Somalia zimeripoti kuwa miripuko miwili ya kutisha ya mabomu pamoja na milio ya risasi imeitikisa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Muhammad Hussein, mmoja wa makanda wa polisi nchini Somalia amenukuliwa akisema kuwa mripuko wa kwanza wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari ulijiri karibu na Wizara ya Kazi, ambapo majengo ya wizara nyingine pia yaliathirika. Kwa mujibu wa Hussein, mripuko mwingine wa bomu ulitokea muda punde baada ya ule wa kwanza na ulifuatiwa na ufyatuaji ovyo risasi uliofanywa na washambuliaji.

Watu wakiokolewa baada ya hujuma za kigaidi nchini Somalia

Hadi sasa bado hasara kamili iliyosababishwa na hujuma hiyo haijatangazwa kama ambavyo hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo, ingawa kidole cha kwanza cha lawama kimeelekezwa kwa wanachama wa kundi la kigaidi la Ash-Shabab, ambalo limekuwa likifanya hujuma kama hizo. Kundi hilo lenye uhusiano na genge la kigaidi la al-Qaidah, hadi sasa ndilo mhusika mkuu wa utegaji mabomu na mashambulio ndani na nje ya Somalia. Tangu mwaka 2007 kundi hilo limekuwa likifanya juhudi zenye lengo la kuipindua serikali kuu ya nchi hiyo ambayo inapata himaya kutoka kwa askari wa Umoja wa Afrika AMISOM.