Mar 27, 2019 16:05 UTC
  • Watu 10 wauawa katika hujuma ya Boko Haram nchini Niger

Watu 10 wameuawa katika shambulizi la bomu la kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram mashariki mwa Niger.

Meya wa mji wa N'Guigmi, Abba Kaya Issa ameliambia shirika la habari la AFP leo Jumatano kuwa, mbali na raia 10 kuuawa, magaidi wawili waliokuwa wamejifunga mabomu pia waliangamia katika hujuma hiyo ya jana jioni.

Amesema mmoja wa magaidi hao alikuwa mwanamke, na kwamba alijiripua nje ya nyumba na askari polisi katika kambi ya polisi iliyoko katika wilaya ya Dileram, kaskazini mwa eneo la Diffa karibu na Ziwa Chad, mpakani mwa nchi hiyo na Nigeria.

Mashuhuda wanasema watu kadhaa wakiwemo watoto wadogo wamejeruhiwa katika shambulio hilo, na kwamba magaidi hao waliteketeza kwa moto nyumba kadhaa katika eneo hilo.

Wanajeshi wa Niger

Shambulizi hilo la jana jioni linaonekana kuwa la ulipizaji kisasi, kwa kuwa limejiri chini ya wiki mbili baada ya magaidi 33 wa kundi hilo la Boko Haram kuuliwa katika operesheni ya vikosi vya nchi hiyo katika mji wa Diffa ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo jirani kabisa na mpaka wa Nigeria.

Kundi hilo la wakufurishaji limekuwa likifanya mashambulizi ya kikatili katika nchi ya Nigeria na majirani zake Niger, Chad na Cameroon, mashambulio ambayo hadi hivi sasa yameshapelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hizo za Afrika Magharibi.

Tags