Apr 02, 2019 13:50 UTC
  • Zaidi ya watu 1000 wamekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu nchini Msumbiji

Viongozi wa idara ya Msumbiji wametangaza kwamba zaidi ya watu 1000 wameambukizwa maradhi ya kipindupindu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo maradhi hayo yameibuka kufuatia mafuriko ya hivi karibuni yaliyosababishwa na kimbunga cha Idai kilichoyakumba maeneo ya katikati mwa nchi hiyo. Taarifa hiyo imeongeza kwamba imesajili majina ya watu 1,052 walioambukizwa na kwamba mtu mmoja tayari amepoteza maisha kwa maradhi hayo. Taarifa zaidi zinasema kuwa licha ya kutolewa misaada mbalimbali kutoka duniani kwenda Msumbiji, lakini bado malaki ya watu walioathirika na kimbunga hicho wanakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kibinaadamu.

Kimbunga na mafuriko nchini Msumbiji

Hii ni katika hali ambayo kuna uwezekano wa ugonjwa wa kipindupindu kuenea zaidi katika maeneo yaliyokumbwa na janga hilo. Kabla ya hapo pia Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea janga la pili la maradhi ya kipindupindu na maradhi mengine nchini humo kutokana na athari ya kimbunga cha Idai.

Aidha shirika hili lilisisitizia udharura wa kutumwa misaada ya haraka kwa ajili ya watu milioni moja na laki nane wanaoishi maeneo yaliyokumba na kimbunga hicho. Kimbunga cha Idai kilitokea tarehe 17 mwezi ulioisha wa Machi kati ya nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na kusababisha uharibifu mkubwa wa kimada na roho za watu.

Tags