Apr 11, 2019 13:58 UTC
  • UN: Watu 56 wameuawa katika mapigano yanayoendelea Libya

Umoja wa Mataifa umesema mapigano kati ya vikosi vya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vile vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar nchini Libya yamesababisha watu 56 kupoteza maisha kufikia sasa.

Aidha umoja huo umetangaza leo Alkhamisi kwamba, mapigano ya hivi sasa ya nchini Libya yanayoonekana kuwa ya kugombania mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli, yameshapelekea watu 6000 wa mji huo kuwa wakimbizi, katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Umoja wa Mataifa umelazimika kuakhirisha mkutano wa amani wa Libya uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 14 hadi 16 mwezi huu wa Aprili baada ya kuzuka mapigano hayo. Mkutano huo ulitazamiwa kujadili na kuandaa ramani ya njia kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

Siku ya Alkhamisi ya tarehe 4 Aprili, Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri kwa wafuasi wake kuushambulia mji mkuu huo wa Libya,  na kuwataka wakazi wa mji huo wajisalimishe kwake. Hata hivyo Fayez Mustafa al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa na jamii ya kimataifa ametoa amri ya kukabiliana na vitisho vyovyote vinavyotolewa na Khalifa Haftar.

Msafara wa vikosi vya Jenerali Haftar

Huku hayo yakiarifiwa, habari kutoka Rome zinaeleza kuwa, Italia ambayo Libya ilikuwa koloni lake zamani imeionya vikali Ufaransa ambayo inamuunga mkono Haftar, dhidi ya kuuunga mkono upande wowote kwenye mapigano hayo.

Duru za kidiplomasia zinaarifu kuwa, serikali ya Paris imezuia kutolewa taarifa ya Umoja wa Ulaya inayomtaka Jenerali Khalifa Haftar aviagize vikosi vyake visitishe mashambulizi mara moja.

Tags