Apr 18, 2019 13:25 UTC
  • WHO: Idadi ya waliouawa katika mapigano ya Tripoli, Libya yapindukia watu 200

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika mashambulizi ya vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar vya kutaka kuudhibiti mji mkuu wa Libya, Tripoli imeongezeka na kufikia watu 205.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo Alkhamisi na WHO imeongeza kuwa, watu wengine 913  wamejeruhiwa katika mapigano hayo ya wiki mbili viungani mwa mji mkuu Tripoli.

Wakati huohuo, Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema watu zaidi ya 20,000 wamekimbia mapigano hayo yanayoendelea kati ya jeshi linalojiita kuwa la kitaifa na la Serikali ya Muungano wa Kitaifa huko Tripoli nchini Libya

Ripoti zinaeleza kuwa kuendelea mapigano hayo pambizoni mwa mji wa Tripoli huenda kukawasha vita vya ndani kama vile vilivyoshuhudiwa  mwaka 2011, ambavyo vilipelekea kung'olewa madarakani na kisha kuuawa kwa Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya.

Gazeti la Wall Street Journal toleo la Ijumaa iliyopita lilifichua kuwa, Khalifa Haftar alipokea kitita cha mamilioni ya dola akiwa safarini mjini Riyadh, kabla ya kuanzisha operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Tripoli

Mapigano hayo mapya yanayoendelea kushuhidiwa nchini humo yalianza tarehe 4 mwezi huu kufuatia safari ya Khalifa Haftar, kamanda wa Jeshi la Kitaifa la Libya nchini Saudia, ambapo mara tu baada ya kurejea nchini humo alitangaza vita dhidi ya Tripoli, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo.

Jenerali muasi Khalifa Haftar ametupilia mbali mwito wa jamii ya kimataifa inayomtaka asitishe mara moja mapigano dhidi ya wapiganaji watiifu kwa serikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli na inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Tags