May 11, 2019 07:44 UTC
  • UNICEF: Wapiganaji watiifu kwa serikali ya Nigeria wawaachia huru watoto 900

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, kundi la wapiganaji wenye mfungamano na vikosi vya serikali ya Nigeria limewaachia huru mamia ya watoto waliokuwa wakitumiwa na kundi hilo katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Mkuu wa UNICEF nchini Nigeria, Mohamed Fall amepongeza hatua ya kundi hilo la wapiganaji kuwaachia huru watoto 900 jana Ijumaa.

Amesema, "Hatua hii inafikisha idadi ya watoto walioachiwa huru na makundi ya wapigajani watiifu kwa serikali ya Abuja kufikia watoto 1,700 na kitendo hiki kinapaswa kutambuliwa na kupongezwa."

Kwa mujibu wa UNICEF, makundi yasiyokuwa ya kiserikali na ambayo yamekuwa yakisaidiana na vikosi vya serikali kukabiliana na Boko Haram yalisajili watoto zaidi ya 3,500 kati ya mwaka 2013 na 2017 huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi. 

Wanachama wa Boko Haram

Oktoba mwaka jana, kundi hilo liliwaachia huru watoto 833 lililokuwa likiwatumia katika vita dhidi ya Boko Haram.

Hii ni katika hali ambayo, huko nyuma UNICEF ilieleza kuwa taasisi hiyo ina wasiwasi mkubwa kutokana na ongezeko kubwa la kutumiwa watoto wadogo hususan wasichana kama 'mabomu watu' na kundi la kigaidi la Boko Haram, huko kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kusisitiza kuwa kuwatumia watoto namna hiyo ni ukatili wa kupindukia.

Tags