May 15, 2019 07:48 UTC
  • Maelfu ya watu wakimbia makazi yao Nigeria kuogopa mashambulizi ya Boko Haram

Maelfu ya wanavijiji wamekimbia makazi yao kaskazini mashariki mwa Nigeria wakikwepa mashambulizi ya kigaidi ya Boko Haram katika mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Maafisa wa eneo hilo wamesema kuwa maelfu ya wakazi wa kijiji cha Molai kilichoko umbali wa kilomita 5 kutoka mjini Maiduguri wiki iliyopita walikimbia makazi yao kukwepa mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram.

Kwa mujibu wa maafisa hao, watu sita wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi ya Boko Haram kwenye kijiji hicho cha Molai ambapo magaidi hao wamechoma moto pia makumi ya nyumba za wakazi wa kijiji hicho.

 

Tangu mwaka 2009, genge la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Tangu mwaka 2015 genge hilo limepanua wigo wa mashambulizi yake hadi katika nchi jirani na Nigeria yaani Niger, Cameroon na Chad.

Zaidi ya watu 20,000 wameshauawa katika jinai hizo za Boko Haram hadi hivi sasa na zaidi ya milioni mbili wengine wamekuwa wakimbizi.

Tags