Waislamu Uganda kuendelea kushinikiza mfumo wa benki za Kiislamu nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53947-waislamu_uganda_kuendelea_kushinikiza_mfumo_wa_benki_za_kiislamu_nchini_humo
Viongozi wa Kiislamu nchini Uganda wamesisitiza kuwa wataendelea kushinikiza utekelezwaji wa mfumo wa benki za Kiislamu nchini humo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 06, 2019 01:48 UTC
  • Waislamu Uganda kuendelea kushinikiza mfumo wa benki za Kiislamu nchini humo

Viongozi wa Kiislamu nchini Uganda wamesisitiza kuwa wataendelea kushinikiza utekelezwaji wa mfumo wa benki za Kiislamu nchini humo.

Viongozi hao walitumia maadhimisho ya Sikukuu ya Idul Fitri kutoa mwito huo ambapo wanasisitiza kuwa watapambana juu chini na watu wanaojaribu kukwamisha utekelezaji wa mfumo huo. 

Katika ujumbe wake wa Idul Fitri, Mufti Mkuu wa Uganda, Sheikh Shaban Ramadhan Mubajje amesema, "Dini yetu hairuhusu riba. Tunahitaji beki za Kiislamu sisi kama Waislamu, sielewi ni kwa nini watu wengine wawashwe na pilipili wasioila."

Naye Sheikh Sulaiman Kakeeto, kiongozi wa harakati ya Tabligh nchini Uganda ametupilia mbali madai yaliyoibuliwa na baadhi ya viongozi wa kidini na kijamii, wanaodai kuwa, mfumo wa benki za Kiislamu utatumika kuimarisha harakati za kigaidi sambamba na kuwalazimisha wasiokuwa Waislamu kujiunga kwa nguvu na dini hiyo tukufu. Amesema, "Dini nyingine zina mifumo yao ya kibenki lakini hatujawahi kufuatilia namna inavyofanya kazi. Kanisa Katoliki lina Benki ya Centenary na Kanisa la Kianglikana lina ushirika mkubwa na Benki ya Equity yenye makao makuu yake kwenye jengo la kanisa hilo."

Wiki iliyopita, Baraza la Pamoja la Wakristo nchini Uganda (UJCC) liliitaka serikali ya Kampala isitishe utekelezaji wa mfumo wa benki za Kiislamu nchini humo, hadi wafahamishwe na wafafanuliwe namna inavyofanya kazi. Muswada wa sheria inayoruhusu mfumo huo ulipasishwa na Bunge la Uganda mwaka 2016. 

Katika baadhi ya nchi, hata wasiokuwa Waislamu wanakumbatia Benki za Kiislamu

Kenya, Tanzania na Ethiopia ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zenye benki na taasisi nyingine za kifedha zinazofuata mafundisho ya Kiislamu. Benki za Kiislamu zinaonekana kuwa kivutio kwa wateja wengi kutokana na uwajibikaji wake unaoenda sawa na mafundisho ya Kiislamu.

Kinyume na benki au mashirika mengine ya kifedha, mashirika ya kifedha ya Kiislamu huwa hayatozi riba kwa mikopo na pia hujizuia kuwekeza fedha za wateja katika sekta au huduma ambazo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu kama vile pombe, kamari, uuzaji wa nyama ya nguruwe nk.