Watu 38 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Mali
(last modified Wed, 19 Jun 2019 03:04:15 GMT )
Jun 19, 2019 03:04 UTC
  • Watu 38 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Mali

Watu wasiopungua 38 wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mapigano ya kikabila nchini Mali.

Serikali ya Mali imetoa taarifa ya kuthibitisha mauaji hayo ya usiku wa kuamkia jana katika vijiji vya Gangafani na Yoro, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Burkina Faso.

Baadhi ya duru nchini humo zimeripoti kwamba watu hao wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyowahusisha watu wa kabila la Dogon, ambao ni wawindaji na mahasimu wao wa kabila la Fulani ambao ni wafugaji. Goundjou Poudiougou, afisa wa serikali katika eneo hilo amesema maiti za watu waliouawa zimetapakaa katika vijiji hivyo viwili. 

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya watu wenye silaha kutekeleza shambulizi la kikatili katika kijiji cha Sobane-Kou, katikati ya nchi hiyo na kuua makumi ya watu wakiwemo watoto wadogo.

Ramani ya Mali

Mapigano hayo pia yalizihusisha jamii mbili hizo ambazo zimekuwa zikihasimiana kwa muda mrefu sasa.

Inafaa kuashiria kuwa, mara kwa mara Mali imekuwa ikishuhidia hujuma za makundi ya wabeba silaha ambazo zimekuwa zikisababisha makumi ya watu kuuawa. 

Mapigano ya kikabila nchini Mali haswa baina ya kabila la kuhamahama la Tuareg na lile la wafugaji la Fulani hadi hivi sasa yameshaua mamia ya watu na kupelekea makumi ya maelfu ya wengine kukimbia makazi yao.