WFP: Mamilioni ya Wakongomani wanakabiliwa na uhaba wa chakula
(last modified Wed, 03 Jul 2019 07:29:46 GMT )
Jul 03, 2019 07:29 UTC
  • WFP: Mamilioni ya Wakongomani wanakabiliwa na uhaba wa chakula

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema mamilioni ya wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanahitajia msaada wa dharura wa chakula katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Msemaji wa WFP, Hervé Verhoosel jana Jumanne alitahadharisha kuwa, iwapo shirika hilo halitapata msaada wa dola milioni 155 haraka iwezekanavyo, wananchi milioni 5.2 wa Kongo DR watakuwa katika hatari ya kufa njaa.

Amesema watu milioni 13 hawana usalama wa chakula katika kona mbalimbali za nchi hiyo, wakiwemo watoto wadogo milioni tano ambao wanakabiliowa na utapiamlo wa kiwango cha juu.

WFP imesema DRC ni nchi ya pili inayokabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula duniani hivi sasa, baada ya Yemen. 

Msemaji wa WFP, Hervé Verhoosel amebainisha kuwa, shirika hilo la Umoja wa Mataifa litaongeza mara tatu kiwango cha msaada wa pesa na chakula kwa wakazi wa mkoa wa Ituri, wanaosumbuliwa na mapigano ya kikabila na ugonjwa hatari wa Ebola.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la UN (WFP)

Claude Jibidar, mwakilishi wa WFP nchini Kongo DR ameashiria mapigano ya kikabila ya hivi karibuni katika mkoa huo, na kusema kuwa vita hivyo vimepelekea watu 160 kuuawa huku mamia ya maelfu ya wengine wakilazimika kuyakimbia makazi yao. 

Mkoa wa Ituri ni katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na virusi vya Ebola, ambavyo hadi kufikia sasa vimeshaua watu 1,400 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.