Jul 21, 2019 12:37 UTC
  • Wazambia waandamana kulalamikia ufisadi wa serikali

Maelfu ya wananchi wa Zambia wamefanya maandamano kulalamikia ufisadi mkubwa wa kifedhi ndani ya serikali ya nchi hiyo.

Maandamano hayo yalishuhudiwa jana Jumamosi katika mji mkuu Lusaka, ambapo waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kuikashifu serikali iliyopo madarakani kwa kuzongwa na kashfa za ufisadi.

Waandamanaji hao walikuwa wamevalia mavazi ya njano, sambamba na kupeperusha mabango ya rangi hiyo, ikiwa ni ishara ya kuipa onyo serikali ya Rais Edgar Lungu wanayoitaja kuwa ya kifisadi.

Baadhi ya waandamanaji hao wamenukuliwa wakilalamika kuwa, mawaziri na maafisa wengine serikali wanaishi maisha mazuri wakimiliki majumba na magari ya kifahari kwa gharama za walipa kodi, ilhali wananchi wa kawaida wanaishi maisha ya kuhangaika.

Rais Edgar Lungu ambaye wapinzani wanamtuhumu kuwa anaendesha nchi kwa mabavu

Mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia alitangaza kujiuzulu wadhifa wake kulalamikia kashfa za ufisadi zinazoizunguka serikali ya Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo.

Itafahamika kuwa, Zambia ni moja ya nchi za Kiafrika ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekumbwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Tags