Rais wa Msumbiji na kiongozi wa Renamo wasaini makubaliano ya amani
(last modified Fri, 02 Aug 2019 01:20:03 GMT )
Aug 02, 2019 01:20 UTC
  • Rais wa Msumbiji na kiongozi wa Renamo wasaini makubaliano ya amani

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji na Ossufo Momade, kiongozi wa Renamo, iliyokuwa harakati ya waasi na ambayo sasa ni chama cha siasa cha upinzani, wamesaini mkataba wa amani wa kuhitimisha uhasama wa vita vya kijeshi.

Viongozi hao wawili walipeana mikono na kukumbatiana baada ya kusaini makubaliano hayo jana Alkhamisi.

Kufuatia kusainiwa makubaliano hayo ya amani, maelfu ya wapiganaji waliosalia wa Renamo watakabidhi silaha zao, zikiwa zimesalia wiki chache kabla ya safari ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis huko nchini Msumbiji na vile vile kabla ya uchaguzi mkuu wa taifa uliopangwa kufanyika katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu; uchaguzi ambao unatazamiwa kuwa kigezo cha kupima maridhiano mapya yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili, ambazo sasa ni washindani wa kisiasa.

Alipohutubia bunge siku ya Jumatano, ambapo alitangaza kuwa sherehe ya kusainiwa makuabliano hayo itafanyika kwenye kambi ya kijeshi ya Renamo iliyoko eneo la mbali la milima Gorongoza, Rais Nyusi alisema: "Makubaliano tutakayosaini yanaashiria kumalizika rasmi mzozo kati ya wapiganaji wa Renamo na vikosi vya ulinzi na usalama, na kuruhusu kupatikana amani ya kudumu, iliyokuwa ikingojewa kwa muda mrefu na Wamsumbiji wote.

Alfonso Dhlakama

Kusainiwa makubaliano hayo ya amani kumehitimisha mchakato mrefu wa mazungumzo ya amani ambayo yalianzishwa na kiongozi wa kihistoria wa Renamo Alfonso Dhlakama, aliyeaga dunia mwezi Mei mwaka jana.

Mnamo katikati ya muongo wa 1970, Renamo iliendesha vita vikali vya ndani dhidi ya serikali ya chama cha Frelimo vilivyosababisha vifo vya watu milioni moja kabla ya mapigano hayo kusita mwaka 1992.

Mapigano mapya baina ya pande mbili yalizuka tena kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.

Mazungumzo kati ya serikali na Renamo yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 2016 na kuendelea hata baada ya kufariki dunia Dhlakama kutokana na mshtuko wa moyo.../