Iran yasisitiza kuimarisha uhusiano wa pande zote na Afrika Kusini
Akizungumza na Balozi iwa Afrika Kusini mjini Tehran, Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuimarisha uhusiano wa pande zote na nchi za bara la Afrika na khususan Afrika Kusini.
Hussein Amir Abdollahian jana alikuwa na mazungumzo na Vika Mazwi Khumalo Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran; ambapo alikutaja kuimarisha uhusiano wa kibunge na kisiasa kati ya maafisa wa nchi mbili kuwa kuna na athari katika kukuza ushirikiano kati ya Iran na Afrika Kusini. Amir Abdollahian ameashiria heshima mahsusi ya wananchi wa Iran kwa mzee Nelson Mandela kama nembo ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ( Apartheid) na kupongeza misimamo ya Afrika Kusini katika matukio ya kieneo na kujielekeza nchi hiyo katika njia za ufumbuzi wa kisiasa.
Msaidizi wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa aidha ameshukuru uungaji mkono endelevu wa Afrika Kusini kwa Palestina na kueleza kuwa: Misimamo hiyo inadhihirisha busara ya kujivunia ya chombo cha siasa za nje cha Afrika Kusini. Amir Abdollahian ameongeza kuwa hatua za kichokozi za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina ambazo ni natija ya mienendo ya kuchupa mipaka ya Rais wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati hazitakuwa na mwisho mwema kwa Uzayuni.
Katika mazungumzo hayo, naye Balozi wa Afrika Kusini mjini Tehran ameshukuru na kupongeza nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Asia Magharibi na ulimwenguni kwa ujumla na kutaka kustawishwa uhusiano kati ya nchi yake na Iran katika nyuga mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kieneo.