Aug 18, 2019 07:51 UTC
  • Ugonjwa wa surua waua maelfu ya watu Congo DR

Shirika la Madatari Wasio na Mpaka (MSF) limeripoti kuwa zaidi ya watu 2700 wameaga dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na ugonjwa wa surua.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imesema kuwa, zaidi ya watu 2700 wameaga dunia Congo DR kutokana na ugonjwa wa surua katika kipindi cha baina ya Januari na Agosti mwaka huu. 

Taarifa ya Shirika la Madatari Wasio na Mpaka imeongeza kuwa, hili ndilo wimbi kubwa zaidi ya vifo vilivyosababishwa na surua katika Jamhuri ya Kidemokkrasia ya Congo tangu ugonjwa huo ulipoikumba nchi hiyo kwenye miaka ya 2011 na 2012. Imesema kuwa watu zaidi ya laki moja na 45 elfu walikuwa tayari wamepatwa na ugonjwa wa surua nchini Congo katika kipindi cha mwezi Januari hadi mwanzoni mwezi huu wa Agosti na wagonjwa 2,735 miongoni mwao wameaga dunia. 

Jumuiya ya MSF inasema kuwa operesheni ya kupambana na ugonjwa wa surua katika Jamhuri ya Kidemopkrasia ya Congo inatatizwa na ukosefu wa bajeti na nguvu kazi kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo. Taarifa ya jumuiya hiyo inasema kuwa ugonjwa huo wa surua umeenea katika mikoa 23 kati ya mikoa yote 26 ya Jamhuri ya Kiodemokrasia ya Congo. 

Waathirika zaidi wa ugonjwa huo ni watoto wadogo wenye umri wa miezi 5 hadi 6 na mabarobaro.   

Tags