Aug 23, 2019 06:57 UTC
  • Kikosi maalumu cha kupambana na magaidi wa Boko Haram
    Kikosi maalumu cha kupambana na magaidi wa Boko Haram

Wanamgambo wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Boko haram wamewateka nyara watu 11 katika eneo moja la kaskazini mwa Cameroon.

Vyombo vya habari vimeripoti habari hiyo na kumnukuu mkuu wa mkoa wa jimbo la kaskazini mwa Cameroon akisema kuwa, watu hao 11 walikuwa ni wasafiri katika basi moja na walikuwa njiani kuelekea katika maeneo ya ndani kabisa ya kaskazini mwa Cameroon, wakati basi lao lilipovamiwa na magaidi wa Boko Haram na kutekwa nyara. 

Kikosi cha nchi nne za Niger, Cameroon, Chad na Nigeria cha kupambana na magaidi wa Boko Haram kimesema kuwa, kuna uwezekano mkubwa watu hao wamepelekwa katika maeneo yaliyo magumu kufika; karibu na Ziwa Chad hivyo itakuwa ni vigumu sana kuwaokoa. Eneo hilo liko baina ya Cameroon, Chad na Nigeria. 

Magaidi wa Boko Haram wana historia ya kuteka nyara raia wasio na ulinzi

 

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilibeba silaha na kuanzisha uasi mwaka 2009 kwa lengo la kuasisi utawala eti wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo mbali na ndani ya nchi hiyo, limepanua wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon. Hadi hivi sasa, zaidi ya watu 20 elfu wameshauawa katika nchi hizo nne za magharibi mwa Afrika na zaidi ya wengine milioni mbili wamekuwa wakimbizi. 

Kushindwa nchi za eneo hilo na hasa Nigeria kuliangamiza kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram kama alivyokuwa ameahidi Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo wakati wa kampeni za uchaguzi, kumedhoofisha mkakati wa kukabiliana na genge hilo.

 

Tags