Vikosi vya Haftar: Hatutaki mazungumzo, mapigano ndiyo njia bora ya suluhu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55877-vikosi_vya_haftar_hatutaki_mazungumzo_mapigano_ndiyo_njia_bora_ya_suluhu
Wapiganaji wa jenerali mstaafu wa Libya, Khalifa Haftar wamepinga mwito wa Umoja wa Mataifa wa kurejea katika meza ya mazungumzo, wakisisitiza kuwa vita ndiyo njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoikabili nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 08, 2019 07:40 UTC
  • Vikosi vya Haftar: Hatutaki mazungumzo, mapigano ndiyo njia bora ya suluhu

Wapiganaji wa jenerali mstaafu wa Libya, Khalifa Haftar wamepinga mwito wa Umoja wa Mataifa wa kurejea katika meza ya mazungumzo, wakisisitiza kuwa vita ndiyo njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoikabili nchi hiyo.

Msemaji wa vikosi hivyo, Jenerali Ahmed al-Mesmari amesema mashambulizi yao yameingia katika hatua za mwisho, na kwamba hawaoni umuhimu wa mazungumzo.

Amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari katika Umoja wa Falme za Kiarabu na kubainisha kuwa, "Wakati bunduki zinazungumza, diplomasia hukimya. Muda wa kurejea katika mazungumzo umekwisha."

Msemaji wa vikosi vya Haftar amesisitiza kuwa, suluhisho la kijeshi ndilo bora zaidi katika kurejesha amani na kudumisha utawala wa sheria.

Jenerali muasi wa Libya, Khalifa Haftar

Haya yanajiri siku chache baada ya Mkuu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusema kuwa wanachama wa baraza hilo wanasisitiza udharura wa kupatikana ufumbuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Libya. Vasily Nebenzya alikiambia kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Usalama kwamba wanachama wote wa baraza hilo wanaafikiana kwamba, mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi, na kwamba uhasama unapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.

Mashambulizi yanayoendelea kufanywa na wapiganaji wa jenerali mstaafu Khalifa Haftar dhidi ya Tripoli tangu mwezi Aprili mwaka huu yamevuruga zaidi hali ya Libya.