Sep 19, 2019 14:28 UTC
  • Boko Haram yaua watu 9 kwa mishale, mikuki na mapanga Nigeria

Watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameshambulia kijiji kimoja huko kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua watu tisa.

Duru za kijeshi zimethibitisha kutokea hujuma hiyo usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Aljilati Ngomari karibu na mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno.

Lukman Rufai, kiongozi wa makundi ya kiraia yanayopambana na Boko Haram na yanayoungwa mkono na serikali ya Abuja amesema baada ya watu tisa kuuawa kikatili na wanamgambo hao kwamba, miili yao ilitupwa katika msitu wa karibu.

Mashuhuda wanasema watu hao waliuawa kwa kulengwa na mishale na mikuki huku wengine wakikatwa mapanga.

Wiki iliyopita, wanachama wa kundi la Boko Haram walishambulia kituo cha kijeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua wanajeshi tisa.

Matakfiri wa Boko Haram

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe harakati zake mwaka 2009, huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na hujuma za genge hilo.

Harakati za Boko Haram kwa sasa zimeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad. Serikali ya Nigeria inalaumiwa kwa kuzembea katika kukakabiliana na kundi hilo la kigaidi.

Tags