Gadi ya pwani ya Libya yaokoa makumi ya wahajiri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56324-gadi_ya_pwani_ya_libya_yaokoa_makumi_ya_wahajiri
Gadi ya Pwani ya Libya imetangaza kuwaokoa wahajiri haramu wapatao 70 baada ya boti yao kuzama katika bahari ya Mediterania.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 29, 2019 23:06 UTC
  • Gadi ya pwani ya Libya yaokoa makumi ya wahajiri

Gadi ya Pwani ya Libya imetangaza kuwaokoa wahajiri haramu wapatao 70 baada ya boti yao kuzama katika bahari ya Mediterania.

Ayoub Gassim, msemaji wa Gadi ya Pwani ya Libya amesema boti hiyo iliyokuwa imejaa kupindukia ilizama katika mji wa magharibi wa Misrata, yapata kilomita 187 mashariki mwa mji mkuu Tripoli ikiwa njiani kuelekea Ulaya.

Awali Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) kupitia ukurasa wake wa Twitter lilitangaza kwamba boti iliyokuwa imebeba wahamiaji haramu 50 imezama baharini na kwamba shirika hilo lipo tayari kutoa msaada kwa wote watakaookolewa.

Shirika la Alarm Phone nalo limetangaza kuwa, boti ya pili imezama katika bahari ya Mediterania ikiwa na wahajiri 56. 

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.

Wahajiri haramu wakijaribu kuokoa maisha yao

Hata hivyo ripoti zinaeleza kuwa, asilimia kubwa ya wahajiri hao huwa hawafiki wanakoelekea, bali huishia mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu, kuzama baharini au kupigwa mnada masokoni na kuuzwa kama watumwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetangaza kuwa, zaidi ya wahajiri elfu mbili waliaga dunia katika bahari ya Mediterania katika mwaka uliopita wa 2018.