Oct 12, 2019 08:08 UTC
  • WHO: Ebola imedhibitiwa katika vijiji vya Kongo DR

Afisa wa ngazi za juu wa Shirika la Afya Duniani WHO amesema juhudi za kuvitokomeza kikamilifu virusi vya Ebola katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kong zinaendelea kuzaa matunda.

Akizungumza mjini Geneva kuhusu hali ya ugonjwa huo kwa sasa nchini DRC, Afisa Mkuu Mtendaji wa Idara ya Dharura ya WHO, Dakta Michael Ryan amesema, "Virusi vya ugonjwa huo sasa vimedhibitiwa katika maeneo ya vijijini vilikogunduliwa mwezi Agosti mwaka jana, na huu ni wakati wa kutokomeza kikamilifu virusi hivyo." 

Amesema kwa sasa virusi vya ugonjwa huo hatari viko katika maeneo ya Mambasa, Kimanda, Beni na Mandima,  katikati ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Chanjo ya Ebola DRC

Afisa huyo wa WHO amebainisha kuwa, changamoto kubwa kwa sasa ni kuwa baadhi ya maeneo hayo yanafikika baada ya kusafiri kwa pikipiki kwa muda wa saa tano, na makundi kadhaa yenye silaha yanaendelea kufanya mashambulizi katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, idadi ya watu walioaga dunia kwa homa hatari ya Ebola imefikia 2014 tangu maradhi hayo yalipuke tena katika nchi hiyo Julai mwaka jana. Aidha kesi za maambukizi ya ugonjwa huo zimefikia 3072.

Tags